13.2.17

Jinsi ya kuactivate akaunti ya Administrator iliyofichwa kwenye Windows 10

BY net tamaduni

Watumiaji wengi wa kompyuta hasa hizi zinazotumia mifumo endeshi ya kisasa kama Windows 10 hawafahamu kama kuna akaunti ya administrator iliyofichwa ambayo inampa mtumiaji uwanja mkubwa wa kukitawala kifaa chake.



Kwa kawaida unapoinstall Windows katika kompyuta yako huwa unapewa akaunti ya Administrator ambayo unaitumia katika matumizi yako ya kawaida kabla hujaamua kutengeneza akaunti nyingine. Napozungumzia akaunti katika mifumo endeshi hasa huu wa windows ni kama chumba chako katika kompyuta hiyo kinachokuruhusu kufanya mambo uliyoruhusiwa tu na kiongozi wako (administrator).
Mfano mzuri ni pale familia inapoamua kuwa na kompyuta moja inayotumika na watu wote kwenye nyumba, mzazi anaweza akaamua kutengeneza akaunti za watoto, za wazazi pamoja na za wafanyakazi na kila akaunti ikawa inajitegemea.
Kwa kufanya hivyo inarahisisha gharama za kununua kompyuta kwa kila mwanafamilia, mara nyingi akaunti za wazazi huwa zina ruhusa za uadministrator hivyo anakuwa na uwezo wa kukagua kila kona ya chombo, watoto na wafanyakazi unaweza ukawapa akaunti za wageni (Guests Account) na wanakuwa na ruhusa chache.
Sasa ukiacha ile akaunti ya administrator ambayo Windows inakupa mara baada tu ya kufanya installation, kuna akaunti nyingine ya administrator ambayo huwa imefichwa, na hii huwa inafaida nyingi sana ukilinganisha na ile akaunti ya administrator unayopewa na Windows moja kwa moja kama wewe ni mtundu unayependa kupata full control ya kompyuta yako.
Akaunti hii itakusaidia kuingia katika kompyuta yako hata kama umesahau password yako, hebu tuangalie njia za kuweza kuifichua akaunti hii.
  1. Bonyeza alama ya Windows katika keyboard yako, kisha andika neno cmd ili kuingia kwenye Command Prompt
  2. Baada ya kuandika, yatatokea matokeo tofauti chagua lile la kwanza lilioandikwa Command prompt kisha Right Click ili uweze kurun kama administrator (Run as administrator)
  3. Baada ya command prompt kufunguka (ukurasa mweusi hivi), andika ‘net user’ ili uweze kuona akaunti zote zilizopo katika kompyuta hiyo
  4. Baada ya hapo andika komandi ‘net user administrator /active:yes’ ili uweze kuruhusu akaunti ya administrator iliyofichwa. Kama unapenda kuruhusu na akaunti ya wageni (Guest Account) unaweza ukaandika komandi hii pia ‘ net user guest /active:yes’
cmd-01
Baada ya hapo akaunti ya Administrator iliyojificha itakuwa tayari ipo wazi na unaweza ukaanza kuitumia bila shaka yoyote. Kumbuka akaunti hii inakuwa haina ulinzi wowote kwa mara ya kwanza hivyo unashauriwa kuweka password ya ngumu ili uweze kuilinda na wadukuzi.
Ili kuipa password, fungua tena command prompt kama administrator alafu andika komandi ‘net user administrator *’, alafu bonyeza enter. Utaletewa sehemu ya kuandika password, hapo andika password unayotaka kisha bonyeza enter. Utaiandika tena kwa mara kwa ajili ya uhakiki. Baada ya hapo akaunti yako itakuwa imelindwa na password.
cmd-02
Kumbuka ukitaka kuzificha tena hizi akaunti tumia komandi , ‘net user administrator /active:no‘ kwa administrator na kwa Guest tumia ‘net user guest/active:no‘.