Samsung kampuni inayofahamika kwa kutengeneza vifaa vya umeme vya aina tofauti yenye makao yake nchini Korea Kusini wameachia SDCard yenye nafasi kubwa zaidi duniani EVO Plus 256GB microSD card.
Kabla ya Samsung SanDisk ilikuwa kampuni ya kwanza kutengeneza SDCard kubwa zaidi yenye uwezo wa 200GB na iliyoteka soko la SDCards duniani kwa kipindi cha mwaka mmoja na nusu sasa.
Ila kwa sasa SanDisk haina budi kushika nafasi ya pili katika orodha hiyo kwa kuwa Samsung imetambulisha EVO Plus yenye uwezo mkubwa zaidi wa 256 GB.
EVO Plus 256GB ina uwezo wa kusoma data wa 95MB/s na uwezo wa kuandika data wa 90MB/s. Hapa naomba tuelewane uwezo wa kusoma na kuandika data wa memeory card ni kitu cha muhimu kwani ndicho kinachosaidia kujua kasi ya kuchukua na kutoa data katika diski hifadhi hiyo.
Diski hifadhi hiyo ndogo imekuja wakati muafaka kutokana na kushamiri kwa drones za kuchukulia video zenye ubora mkubwa wa 4k au kamera za HD za mashine za VR.
Kwa ukubwa iliokuwa nayo diski hii inaweza ikahifadhi video ya 4K ya masaa 12, video ya HD ya masaa 46 na picha takribani 55,000. Diski hii pia inaweza kutumika katika smartphones na vifaa vingine kama tablets.
Diski hiyo itaanza kuuzwa rasmi mwezi June katika nchi 50 duniani kote huku mataifa ya China, Ulaya na Marekani yakiwa yanaongoza katika orodha ya nchi zitakazopata diski hizo mapema.