Kila mmoja wetu hasa kama wewe ni mtumiaji wa kompyuta au simu za kisasa (smartphones) utakuwa sio mgeni wa software (zanatepe) za antivirus. Kama jina linavyojieleza software hizi ni maalumu kwa ajili ya kupambana na virusi vya kompyuta au simu.
Hebu tuangalie kwanza njia ambazo virusi wanavyoweza kuingia katika mfumo wa kompyuta yako;
- Kupitia kwenye vifaa vya kuhifadhi data vinavyochomekwa kama USB Flash Drive na SDCards.
- Kupitia kwenye mtandao kama komyuta yako imeunganishwa na mtandao moja kwa moja
- Kupitia katika viambatanishi vinavyotumwa na barua pepe
Hapa inategemea sana na aina ya virusi aliyeingia katika kompyuta yako na lengo la tengenezaji wa hivyo virusi katika kufanikisha lengo analotaka. Kulingana na aina ya mashambulizi na madhara wanayoleta virusi hawa wamegawanywa katika makundi tofauti tofauti kama Virus, Spyware, Worms, Trojans na Adwares.
Virus wao wanafanya kama jina lao linavyoelekeza, kama walivyo virusi wa wanyama na virusi hivi vya kompyuta vinadhorotesha utendaji wa kompyuta yako kwa kufuta baadhi ya mafaili ya programu au data katika kompyuta yako. Wengine hujiongeza wenyewe na kujaza nafasi ya kompyuta yako hivyo kushusha ufanisi.
Spyware ni aina ya virusi vya kompyuta vinatengenezwa kwa lengo la kuiba data za mtumiaji wa komyuta. Mara nyingi spyware zinajihusisha na masuala kama ya kuiba passwords, pin na baadhi ya mafaili waliyoelekezwa. Spyaware hutumika sana na wadukuzi na mashirika makubwa ya kijasusi katika kufuatilia nyendo za mtumiaji wa kompyuta husika.
Worms kwa lugha ya kiswahili ni minyoo, kama ilivyo minyoo ya binadamu worms wanatekeleza mashambulizi yao katika kompyuta kwa kujiongeza na kujaza nafasi ya kompyuta bila mtumiaji wake kufahamu, mara nyingine worms wanatafuna (futa) baadhi ya mafaili na kuharibu kabisa mwenendo wa kawaida wa kompyuta.
Trojans wao ni kama virusi wanaotumwa kufungulia mlango mashambulizi mengine. Mara nyingi trojans wanaingia wakiwa katika baadhi ya software au viambatanisho vya katika barua pepe tunazopakua kila siku mtandaoni. Mara nyingi hujifanya kama software za nyongeza au za bure na zinakushawishi kuzipakua.
Adwares haw ni virus wa kompyuta wenye lengo la kutangaza biashara za makampuni fulani na mara nyingi wanapatikana katika mitandao. Adwares husumbua sana watumiaji wa vivinjari kama internet explorer na Mozila Firefox kwa kujaza matangazo katika kurasa za tovuti unazotembelea.
Baada ya kuona jinsi virus wanavyoshambulia kompyuta zetu nadhani ni muhimu pia kufahamu jinsi programu za antivirus zinavyopambana navyo. Kuna aina nyingi sana za antivirus katika soko kwa sasa na nilishawahi kuandika hapa programu bora zaidi za antivirus katika soko kwa sasa kama Bitdefender, Kaspersky, Norton na nyingine nyingi.
Interactive: Katika njia hii programu ya antivirus huwa inafanya kazi nyuma ya pazia muda wote na inahakiki kila kitu kinachofanywa na kompyuta muda wote na kuikinga na madhara yanayoweza kuletwa na virusi. Mara nyingi njia hii inapambana zaidi na virusi vinavyoingia kwenye kompyuta kupitia katika mtandao au vifaa vinavyochomekwa.
Scan: Katika njia hii programu ya antivirus inapekua kila sehemu ya kompyuta kuanzia katika diski hifadhi mpaka katika memory na kuangalia dalili zozote za kuwepo kwa madhara au virusi vya kompyuta. Pale inapovikuta huwa inampa taarifa mtumiaji na kumpa njia tofauti za kuweza kuwaondoa au kupambana na virusi hivyo.
Mambo muhimu ya kuzingatia wakati unatumia Antivirus
- Kumbuka kuupdate (kuboresha) programu ya antivirus mara kwa mara kwa kuwa kila siku virusi vipya vinatengenezwa na kinga mpya dhidi ya virusi hivyo pia hutengenezwa
- Pendelea kutumia Antivirus za kulipia kwa sababu zinakuwa na uwezo mkubwa zaidi ukilinganisha na zile za bure
- Kuwa makini unapofuta faili au programu iliyoshambuliwa na virusi kwa sababu unaweza futa mafaili yako ya msingi au mafaili ya programu endeshi
- Hakikisha unairuhusu programu yako ya antivirus kuscan vifaa vyote unavyochomeka katika kompyuta yako kabla ya kuvifungua